Rais Magufuli Apigilia Msumari Sakata la Zanzibar..Adai Hakuna Jinsi zaidi ya Kurudia Uchaguzi
Rais John Magufuli amesema kuwa hana mamlaka yoyote ya kuingilia suala la uchaguzi wa Zanzibar.
Rais Magufuli aliyaeleza hayo jana katika hotuba yake kwa mabalozi
mbalimbali wanaoziwakilisha nchi zao hapa Tanzania iliyosomwa kwa niaba
yake na waziri wa mambo ya nje, ushirikiano wa Afrika Mashariki, kikanda
na kimataifa Balozi Augustine Mahiga jana ikulu jijini Dar es salaam.
Katika hotuba hiyo, Rais Magufuli aliwaeleza mabalozi hao kuwa licha ya
Tanzania kuwa nchi moja, Zanzibar ina mfumo wake wa siasa, ina serikali
yake, Katiba yake na pia tume yake ya uchaguzi inayojitegemea.
Alisema tume hiyo ilifuta uchaguzi kutokana na mapungufu yaliyojitokeza
kisiwani Pemba, na kwamba tayari tarehe mpya ya uchaguzi wa marudio
imekwisha tangazwa kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar.
Alosema mazungumzo ya kutatua mgogoro huo yalifanyika bila mafanikio
ambapo chama kikuu cha upinzani (CUF) kimeendelea kupinga uchaguzi wa
marudio huku vyama vingine kikiwemo chama tawala vikionesha uhitaji wa
uchaguzi huo wa marudio.
Alisema kwa hali ilivyo, busara inahitajika ili kunusuru suala hilo, na
kwamba kususia uchaguzi siyo suluhu bali kutumia nafasi iliyopo sasa
kujadili namna ya kuufanya uchaguzi wa marudio kuwa huru na wa haki.
Aliwaeleza mabalozi hao kuwa serikali pamoja na watanzania walio wengi
wangependa kuona CUF inathibitisha madai yake ya kushinda uchaguzi huo
kupitia sanduku la kura katika uchaguzi wa marudio.
“Tunakiasa chama cha CUF kama ambavyo watanzania wengi wangependa kuona,
kuthibitisha madai ya ushindi wao katika sanduku la kura, hakuna jinsi
nyingine ya kutatua suala hili zaidi ya kukubali kufanya uchaguzi wa
marudio”ilisema sehemu ya hotuba hiyo.
Magufuli amewahakikishia mabalozi hao kuwa nchi ni salama na hali ya
amani na utulivu ni ya kuridhisha katika kipindi hiki cha kuelekea
katika uchaguzi wa marudio.
0 comments