Mwanamke wa Kikurya Apokonya Majambazi Matatu Bunduki Aina ya SMG
Mwanamke wa kitongoji cha Buriba, kata ya Sirari, wilayani Tarime,
anayejishughulisha na biashara ya kuuza kibanda cha duka, Sophia Manguye
(46), amefanikiwa kuwanyang'anya majambazi watatu bunduki moja aina ya
SMG yenye risasi 27, baada ya kupambana nao ndani ya kibanda chake cha
biashara.
Majambazi hayo kabla ya kunyang'anywa bunduki, yalifanya uporaji katika
vibanda kadhaa vya maduka na kufanikiwa kujikusanyia zaidi ya Sh.
180,000, pamoja na vocha za simu za mkononi kutoka maduka matatu
tofauti.
Jambazi aliyeporwa bunduki hiyo na Sophia ni Gesanta Matinde (19), mkazi
wa kijiji cha Kebeyo, kata ya Mbogi, ikiwa na risasi 27.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tarime/Rorya, Gemini Mushi, jana alisema tukio
hilo la uvamizi na unyang'anyi kwa wafanyabiashara lilitokea juzi saa
2:00 usiku katika kitongoji cha Buriba, mji mdogo wa Sirari, baada ya
majambazi watatu waliokuwa na silaha aina ya SMG namba UK 5115 kuwavamia
wafanyabiashara hao.
“Awali majambazi hao waliingia duka la Zaituni Magasi lililopo jirani na
la Sophia na kupora fedha taslimu Sh. 100,000 kabla ya kuingia dukani
kwa Sophia na kupora 80,000 za mauzo, lakini hawakuridhika na kiasi
hicho, hivyo kuingia ndani na kuanza kutafuta fedha nyingine,” alisema
Kamanda Mushi.
Hata hivyo, Kamanda Mushi alisema wakati wakiendelea kupekua kutafuta
fedha nyingine, mwanamke huyo alimvamia jambazi aliyekuwa na silaha
kisha kumng’ang’ania kwa nguvu, huku akipiga kelele za kuomba msaada
hadi walipojitokeza wananchi na polisi waliokuwa karibu kutoa msaada.
Kamanda Mushi alisema baada ya tukio hilo, majambazi wawili walifanikiwa
kutoroka, huku mwanamke huyo akipata majeraha usoni na mikononi wakati
wa kupambana na majambazi hao.
Alisema Jeshi la Polisi limempongeza mwanamke huyo kwa ujasiri
aliouonyesha pamoja na wananchi waliojitokeza na kuongeza nguvu na
kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa na bunduki hiyo ambayo ingeleta madhara
makubwa kwa wananchi.
Aliwaomba wananchi kushiriki ulinzi shirikishi kwa kutoa taarifa za uhalifu kwa jeshi hilo mapema kabla ya matukio.
Alisema kwa sasa wanaendelea kumhoji mtuhumiwa na wengine wawili
waliotoroka wakitafutwa ili waweze kufikishwa katika vyombo vya sheria
Category: habari
0 comments